Tuesday, 22 October 2013



JUMA MWAMBUSI;
MTAALAM WA MBEYA CITY

                                        KOCHA JUMA MWAMBUSI 
   
     Kila mpenda soka Tanzania sasa hivi lazima anaijua timu ya Mbeya City,na wanaijua si kwa vile inashiriki tu ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara,lakini kutokana na kiwango cha hali ya juu kinachoonyeshwa na timu hiyo.Wanakaba kwa pamoja,wanashambulia pamoja na wanashirikiana kwa kila hali wakiwa uwanjani,hilo limezisumbua sana timu pinzani  kila wanapokutana nazo.
            Yote hayo yanafanikiwa kutokana na ubora wa kocha anaefundisha timu hiyo,Juma Mwambusi,kwani anakazania sana soka la kushirikiana. “sipendi timu ninayofundisha iwe na nyota mmoja au wawili na kuwameza wachezaji wengine,huwa nawatayarisha wachezaji wangu wote wawe nyota,wategemeane na washirikiane  kiasi hata mmoja  asipocheza aingie ambae ana kiwango kile kile kama cha  wengine”alisema  Juma Mwambusi alipoongea na mbeyamaskan’ “nina wachezaji wengine zaidi ya kumi na nane wana kiwango sawa sawa na hawa wanaocheza sasa hivi,hivyo sitegemei timu yangu iwe kama nguvu ya soda,tumejipanga vizuri”.

              Akaendelea “Unajua siri ya kua mchezaji mkubwa  na mzuri ni nidhamu,kweli wapo wachezaji wengi duniani wenye nidhamu mbovu na lakini ni mahiri na maarufu sana katika soka,nidhamu ninayoisema mimi ni ile ya kupenda na kuheshimu kile unachokifanya,kufika kwa wakati mazoezini, kufanya mazoezi kwa bidii pale unaposimamiwa na hata ukiwa peke yako,na kujifunza kwa bidii kile kinachokushinda ukiwa uwanjani,na hata unachokiweza kukifanyia mazoezi zaidi ili kisije kukutoka,hiyo ndio nidhamu ninayoisema,”aliongeza.
                                              KOCHA MWAMBUSI

        Juma ambae ni mpole na mcheshi sana akiwa katika maisha ya kawaida,lakini ni mkali na makini sana anapokua katika kazi yake ya ukocha aliendelea“Ili timu iwe na mshikamano lazima kocha uwe na msimamo,usipende kua mkali sana kila mara ili wakuogope,hapo watakua na nidhamu ya uoga na ni rahisi sana kukutania na kutokua makini pindi unapowapa mgongo,na haitakiwi uwe mpole kwani watakua huru sana na mwisho wa siku wote mtaonana mko sawa,kutakua hakuna kiongozi tena”aliendelea kunambia.
     “Kwa hiyo siri yangu kubwa sana ni nidhamu,nataka mchezaji ninaemfundisha ajue anataka nini,ajue anatakiwa afanye nini na pia nataka ajali anachokifanya,hapo tutakua sawasawa,na nina hakika mchezaji mwenye nidhamu lazima atafika mbali sana tofauti na wasio na nidhamu.”
    Juma Zakaria Mwambusi alizaliwa mkoani Mbeya na kupata elimu yake hapo hapo Mbeya,Alipomaliza High School akaanza taratibu kujiingiza katika kozi za awali za ukocha zilizokua zikitolewa na FAT hadi TFF na kupata vyeti kadhaa,haikutosha akaamua kwenda Ulaya ili kuongeza ujuzi na mwaka 2001 akapata DIPLOMA nchini Hungary,na baadae akapata tena DIPLOMA ya kua instructor iliyotolewa na shirikisho la osoka ulimwenguni,FIFA hapa hapa Dar,na mwaka jana amefanya kozi na kufanikiwa kupata licence B ya CAF.hivyo si kocha wa kubahatisha ni kocha aliesomea.
                 Timu alizowahi kufundisha kwanza kabisa ni TUKUYU STARS mwaka 2002 na kufanikiwa hadi kufika katka timu nane bora  na yeye akachaguliwa kuwa ni kocha bora,vilevile TUKUYU STARS ikachaguliwa kua ni timu yenye nidhamu.
Mwaka 2003 akaifundisha timu ya PALSON ya Arusha nayo pia ikaingia hadi nane bora.Na mwaka 2005 alikua ndie kocha wa timu ya mkoa wa Mbeya ya Mapinduzi Stars na wakafanikiwa kuchukua kombe la taifa,mwaka 2007/2008 alikua ni kocha wa timu ya PRISON ya Mbeya,wakashika nafasi ya pili katika ligi kuu na pia akachaguliwa kua ni kocha bora,na mwaka 2001 akawa tena kocha wa timu ya mkoa wa Mbeya Mapinduzi Stars na wakafanikiwa kutwaa ubingwa wa taifa na pia akachaguliwaa kua ni kocha bora wa mashindano.
                                              JUMA MWAMBUSI
           
    Sasa hivi ni kocha wa Mbeya City,timu ambayo tayari imeonyesha sura tofauti ya mchezo wa soka hapa Tanzania,kwani walipoanza mchezo wa kwanza walitoka sare na Kagera,wakaja kuifunga Ruvu Shooting kisha wakatoka sare na Yanga ,wakatoka tena sare na Mtibwa,Simba,Coastal Union,na baadae wakazifunga Oljoro,Rhino,Mgambo na Ruvu JKT.na kila siku timu inazidi kuonyesha ukomavu na kuzoea mikiki mikiki ya ligi kuu.
                                    MWAMBUSI AKIWA NA MSAIDIZI WAKE.


         Alipoulizwa kama wana nia ya kuchukua ubingwa wa Tanzania alisema “tunataka  twende hatua kwa hatua,tunajitayarisha tu na mchezo unaokuja  mbele yetu,hivyo tukifanya vizuri katika huo mchezo tunaanza kujitayarisha na mchezo unaofuata,hatutaki kujichanganya na mambo mengi wakati kuna kazi kubwa ya kufanya hivyo tukifanikiwa kuzifunga timu tunazokutana nazo basi na ubingwa utakuja,lakini sio kazi ya kusema tu kwa mdomo kwamba nataka kua bingwa,inabidi ifanyike sana kazi,sasa hivi nimeanza kupata wasiwasi na waamuzi wanaochezesha hii ligi,sijui kama ni kwa makusudi au kutokujua lakini maamuzi yao mengi yanakua ni ya mashaka.mfano tulifunga goli zuri sana siku tumecheza na Mgambo lakini kwa maajabu mwamuzi akalikataa,hadi leo sijui sababu ya kulikataa hilo goli,hivyo kuna kazi kubwa sana mbele zaidi ya huku tulikotoka,ila nawashukuru sana wapenzi wa soka jijini Mbeya,wanatupa sapoti kubwa sana kiasi kila siku tunajiona tuna deni la kuwalipa,na kuwalipa ni sisi kujitahidi kucheza vizuri na kushinda michezo yetu,nawashukuru sana wachezaji wangu,kwani wamekua wasikivu mno na wamefanikiwa kucheza vizuri hata katika mechi zenye presha kubwa,kwa hilo wanastahili sifa”alimalizia Juma Mwambusi.

No comments:

Post a Comment