David buruan
city no one
Katika michezo iliyochezwa ya ligi kuu ya
Vodacom msimu huu,mechi inayosemekana kwamba ilikua ni nzuri kuliko zote ni kati ya Azam na Mbeya
City iliyochezwa katika uwanja wa Azam chamazi Dar.
Inakumbukwa na wengi kutokana na ubora
wa mchezo ulioonyeshwa na timu zote mbili, kila timu ilionyesha kiwango cha hali
ya juu sana kiasi hata sare iliyopatikana ya magoli 3-3 iliwaridhisha mashabiki
wote.
Katika mchezo huo, nyota wa mchezo kwa
upande wa Mbeya City alikua ni golikipa
wa timu hiyo, David Buruan, kwani pamoja na kufungwa magoli matatu lakini
aliokoa magoli mengi mno. Aliokoa mara mbili akiwa uso kwa uso na mshambuliaji
hatari wa timu hiyo John Boco,akaokoa mara moja akiwa anatazamana na Joseph
Kimwaga, na hizo zote washambuliaji hao walikua wamewapita mabeki wote au kwa
kuwafikiria wameotea au kupigiwa pasi nzuri za mwisho, lakini David aliweza kuwasoma na kuingia
ndani na kucheza kama mlinzi wa mwisho na kuokoa hatari zote hizo.
Hata faulo iliyowapatia Azam
goli la kwanza, alikua ametoka na kwenda kumkabili Joseph Kimwaga aliyewachomoka mabeki wa City na bahati mbaya wakati akijaribu kuokoa akaushka
mpira na kuzaa hiyo faulo.
David alizaliwa mkoani Kigoma na
kupata elimu yake mkoani Iringa,alianza kucheza mpira toka akiwa katika shule
ya msingi Wilolesi mkoani Iringa na kwa vile kipaji chake hakikujificha aliweza
kuchukuliwa mara kadhaa na timu za
mitaani na baadae akachukuliwa kabisa na timu ya Polisi Iringa.
Na wakati akiwa Polisi Iringa, timu ya
Simba ilifanya ziara mkoani Iringa na wakacheza na Polisi, na David akaaminiwa
kua ni kipa katika mchezo huo na akafanya vizuri sana. Na hiyo ndio ilikua mechi yake kubwa ya kwanza.
Baada ya hapo akachukuliwa na timu
ya Tanzania Prisons, huko akacheza kwa mafanikio makubwa hadi akachaguliwa kua ni kipa bora wa ligi kuu ya Vodacom msimu wa 2012/2013.
Na timu ya Mbeya City ilipopanda daraja,
kocha wa timu hiyo Juma Mwambusi aliamua kumchukua na kuwa ndio kipa namba moja
wa timu hiyo.
Na katika michezo yote
aliyocheza ya ligi kuu msimu huu ameonyesha kiwango kikubwa na kumfanya awe ni
mmoja kati ya makipa wazuri hapa Tanzania, ana uwezo mkubwa sana wa kuwasoma
maadui na kuwapanga mabeki wake,na mara nyingi anaanzisha move haraka pale wanapokua wameshambuliwa na akiudaka mpira
anajua mahali pa kuupeleka. Pia ni mzuri sana kucheza krosi na mipira ya
adhabu,hivyo kuwafanya walinzi wake kutulia kila anapokua golini.
Alikua ni kikwazo siku Mbeya City walipopambana
na Yanga jijini Mbeya na kutoka sare ya 1-1, na akaonyesha kiwango cha juu
walipocheza na Simba jijini Dar es salaam na
hata katika mchezo mgumu na Tz Prisons jijini Mbeya alikua katika
kiwango bora sana cha mchezo.
Kwa kiwango alichokionyesa katika misimu
hii miwili, alipokua na Tz Prisons na sasa Mbeya City, siwezi kuja kushangaa
siku atakapochukuliwa katika timu ya taifa ya Tanzania, na nina uhakika
akichukuliwa tu lazima atakua ni Tanzania one, na hatoki tena……






No comments:
Post a Comment