Monday, 3 February 2014

 Mbeya city tunasonga mbele

Timu ya Mbeya City,imepoteza mchezo wake wa kwanza wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania baada ya kufungwa goli moja kwa bila na Yanga katika mchezo uliochezwa jumapili.

Goli pekee lilifungwa na Mrisho Ngasa baada ya kukutana na mpira wa krosi krosi uliookolewa kwa kichwa na beki wa City Yusuf Abdallah na kumkuta Ngasa aliyeusogeza na kupiga kiki iliyoingia pembeni mwa goli laMbeya City.

 Katika mchezo huo Mbeya City walijitahidi  kutafuta goli la kusawazisha lakini ilikua ni ngumu sana kwani kwa muda wote wa kipindi cha pili kuanzia dakikaya 47 walicheza pungufu baada ya kiungo wao mzoefu Steven Mazanda kutolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi wa pambano  hilo.

     Baada ya mchezo,kocha watimu ya Mbeya City Juma Mwambusi alisema timu yake ilifungwa kutokana na kucheza pungufu kitu ambacho ni kigumu sana kwa timu yoyote ya hapaTanzania ukichukulia  unacheza na timu kama Yanga lakini akasema hayo yamepita sasa hivi wanatazama mchezo unaofuata, kwani vita bado sana kuimaliza.
     Akiongelea  kadi aliyopewa Mazanda, kocha Mwambusi alisema “mwamuzi ilitakiwa amuonye, kwani tayari alikua na kadi ya njano,kawaida mwamuzi anatakiwa amwambie kwamba hili ni onyo la mwisho,ukirudia tena utapata kadi nyekundu,lakini yeye aliitoa moja kwa moja kama vile alikua akisubiri afanye hicho kitendo ili amtoe, lakini huo ndio mpira wetu na hao ndo waamuzi wetu, sitaki kabisa kulalamika kuhusu maamuzi yake kwani nitakua  najirudisha nyuma,yaliyotokea tayari yametokea tunasonga mbele”
       Kwa ujumla timu ilicheza vizuri vipindi vyote viwili, ingawa alipotolewa Mazanda mipango ikabidi ibadilishwe.  Deus Kaseke  anayeshambulia kupitia pembeni kushoto , ikabidi aingie katikati kusaidia viungo, hivyo kumfanya Hassan Mwasapili aliyezoea kukaba na kushambulia acheze sana nyuma ili aweze kuwadhibiti Ngasa na Msuva. Ukichukulia mashambulizi mengi ya Mbeya City hua yanaanzia upande wa kushoto, hali hiyo iliathiri kidogo mashambulizi mengi kuelekea golini  mwa Yanga.

      Kwa wachezaji mmoja mmoja kila mmoja alijitahidi sana kucheza kwa uwezo wake wote, ingawa  beki Yusuf Abdallah ndio alikua nyota upande wa  Mbeya City, kwani aliweza kuwamudu vilivyo washambuliaji wa Yanga.
     Ukitazama mchezaji mmoja mmoja utaona kila moja alitimiza majukumu yake kama alivyopangiwa..
 - David Buruan alionyesha ukomavu wake kwani mara kadhaa aliokoa hatari na alikua akiwapanga mno mabeki wake…..
- John Kabanda   aliweza kumzuia sana David Luhende ingawa krosi iliyokuja kuzaa goli ilitokea upande wake lakini si kwamba alikua kakosea ni bahati mbaya beki aliyekuja kuosha  mpira ukamkuta Ngasa. Kabanda alipiga krosi kadhaa langoni mwa Yanga ingawa hazikuzaa magoli.ila alicheza vizuri sana.
 - Hassan Mwasapili kama kawaida alicheza vizuri sana ingawa kadi aliyopewa Mazanda ilimuathiri zaidi yeye kwani mara nyingi yeye pamoja na Deus Kaseke wamezoea kushambulia na kukaba kwa pamoja, hivyo Kaseke alipoingia katikati  kazi kubwa aliifanya peke yake, alifanikiwa kwa kiasi kikubwa.
-Deogratius Deo Julius alicheza kwa utulivu wa hali ya juu, kwani alimficha muda mwingi wa mchezo Didier Kavumbagu, na hakua na papara wakati wa kuokoa hatari nyingi zilizokuja langoni mwa Mbeya City.
-Yusuf Abdallah, kwangu mimi naona alikua ni nyota wa mchezo upande wa City, alikua na timing nzuri za kuokoa mipira na mara nyingi alikaa mbele ya washambuliaji wa Yanga kila mpira unapopigwa kuelekea golini mwa City. Aliiwahi mipira mingi na alifanya “tackling” nyingi zenye mafanikio, pia alicheza mipira mingi sana  ya juu…. Kiujumla alikua nyota .
-Anton Matogolo alipakamata katikati , ingawa dakika za mwanzo alikua taratibu sana lakini baadae alibadilika na alipotolewa Mazanda alifanya kazi kubwa sana ya kunyang’anya mipira na kupiga pasi ndefu nyingi…nadhani aliongoza upande wa City kwa kupiga pasi nyingi.alikua anajua timing za kuwafata kina Domayo na Niliyonzima.
-Peter Mapunda ni mmoja wa hazina za Mbeya City, kwani aliweza kuipenyeza mipira kila mara kwa washambuliaji wa katikati. Ana kasi na pia anapiga chenga huku akimfata beki…..uko vizuri sana Peter..
-Steven Mazanda- nadhani mwamuzi alimchagua mtu wa kumpa kadi nyekundu, kwani  Mazanda alikua akitoa pasi na kuwatuliza viungo wa Yanga. Ukitazama toka mpira unaanza hadi anatolewa alipoteza pasi si zaidi ya mbili, na alikua kila mara anaigawa mipira katika njia ambazo ni ngumu kutokufika.mwamuzi alifanya kitu kibaya sana kumtoa mtaalamu huyu.
-Paul Nonga alikua akiwasumbua sana mabeki wa Yanga, alikimbizana nao na pia alikua akiisogeza mipira anakotaka ingawa nae aliathirika sana na kutoka kwa Mazanda.
- Mwagane Yeya-siogopi kusema kwamba huyu ndie mshambuliaji wa kweli Tanzania. Nadir Haroub na  Kelvin Yondani hawakwenda mbele hata mara moja kama ilivyo kawida yao katika michezo mingine, walitulia na kujaribu kumdhibiti ingawa ilikua ni kazi ngumu sana. Aliicheza mipira yote ya juu na alikua ni tishio  kila anapoupata mpira, ni kwa vile bado alikua hajapona vizuri majeraha yake ndio maana kocha akamtoa kipindi cha pili mwishoni na kuwapa ahueni mashabiki na walinzi wa Yanga. Anajua sana huyu ticha.
-Deus Kaseke – nadhani mwenye jibu zuri la jinsi Kaseke alivyocheza ni Mbuyu Twite, kwani alisumbuliwa sana na sikushangaa kocha  anamtoa na kumuingiza JumaAbdul, Deus alikua akimtoka Twite na mabeki wenzake kama anavyotaka. Ni mmoja kati ya vipaji adimu sana hapa Tanzania. Kila mara anatia njaa na kuwafanya mabeki wa Yanga kulaumiana muda mwingi wa mchezo. Hali ilibadilika kidogo alipoingia katikati kwani ikabidi acheze kwa nguvu sana ili kuweza kuhimili viungo wa Yanga lakini kwa ujumla alimudu sana kazi hiyo.
    Waliokuja kuingia  Saad Kipanga, Richard Peter na Yusuf Wilson nao walicheza vizuri mno ingawa hawakupata muda mrefu lakini ki ujumla hii inaonyesha Mbeya City ina wachezaji wengi sana wenye  viwango vinavyolingana…
      Kwa sasa hivi timu inasonga mbele na kusubiri mchezo unaokuja…..


No comments:

Post a Comment