Friday, 7 February 2014

David buruan;
Kila mchezo unaokuja ni fainali

Kipa wa timu ya soka ya Mbeya City ya jijini Mbeya, David Buruan amesema sasa hivi wanajipanga ili kila mchezo watakaocheza uwe kama ni fainali, hivyo wapo makini sana kuhakikisha wanapata pointi tatu katika kila mchezo.

       “Kwa sasa hivi timu yetu pamoja na uchanga wake,  imekua ni kama zile timu mbili kubwa zinazojulikana hapa nchini, kila tunakokwenda tunakuta timu zimepania ili kuweza kutufunga, hivyo na sisi tumeamua tusibweteke , tufanye kazi zaidi ya mwanzo ili kuhakikisha tunafanya vizuri” alisema kipa huyo.

          “Miaka iliyopita, timu zilikua zikiwekwa kambini  pale tu zinapotaka kucheza na Simba au Yanga, na hata Simba  na Yanga zilikua zikiweka kambi pale tu zinapotaka kukutana zenyewe, lakini kwa sasa ni tofauti, hata Yanga pamoja na kua walikua na kambi nzuri nje ya nchi. Lakini walipokaribia kucheza nasi wakaweka tena kambi  Bagamoyo, hiyo inadhihirisha kwamba  wanatuchukulia kwa tahadhari kubwa, na sisi  inabidi tuzidishe juhudi zaidi ya zile za siku za nyuma” aliongeza David Buruani ambae msimu uliopita ndio alikua kipa bora wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania.

             “Kila mmoja katika timu yetu anajua wajibu wake, hivyo ni rahisi kufikia malengo pale tunapojiwekea na kwa sasa hivi malengo yetu ni kuhakikisha hatupotezi pointi katika michezo inayokuja” aliongeza David.
        Kuhusu mchezo na Yanga walipoteza kwa goli moja anasema “  ule mchezo umepita,  nashukuru wachezaji wote wamekwishasahau kuhusu huo mchezo, wamehamisha akili zote katika hii mingine nayokuja mbele, tunaomba Mungu atusaidie tukichanganya na juhudi zetu tuna uhakika tutafika mahali ambapo  tunataka kufika”alisema.

     Na kuhusu mashabiki wa Mbeya City akasema “Sio siri. Mafanikio yetu kwa asilimia kubwa yanaletwa  kutokana na hamasa inayoonyeshwa na mashabiki wetu, wanatufuata kila tunapokwenda na hilo halijawahi kutokea katika hizi nchi za Africa, kwetu sisi tunaona kama ni deni na kulipa kwake ni kujituma ili kupata ushindi. Hua naona raha sana kila ninapokua uwanjani nikitazama nje mashabiki wa timu yetu wanakua wamewameza mashabiki wa timu pinzani….mfano uliona siku tumecheza na Azam na pia siku tumecheza na Yanga, ilikua kama tuko nyumbani uwanja wa Sokoine, mashabiki walikua wanashangilia kuanzia mwanzo wa mchezo hadi mwisho na kutufanya tupate ujasiri zaidi wa kupambana, tunawashukuru  sana mashabiki wetu, tutajitahidi tusiwaangushe” alimalizia David Buruani.
               picha zote kwa hisani ya David Baruan.imeandikwa na Abdul Sudi,Mbeya.

             

No comments:

Post a Comment