Mbeya city walivyopambana na simba
Mbeya City wamefanikiwa kutoka
sare ya goli moja kwa moja na timu ngumu ya Simba iliyocheza kwa kiwango cha
juu sana kuonekana hivi karibuni. Katika mchezo huo Simba walionekana
kujaribu kumiliki kila idara na kuwafanya Mbeya City muda mwingi kujitahidi kuharibu mipango ya Simba.
Mchezo huo ulikua ni wa kiufundi zaidi na
sifa za mwanzo ziwaendee makocha wa timu zote mbili kwa jinsi walivyoingia
katika huo mchezo.
Kocha Juma Mwambusi alibadili kidogo aina
ya uchezaji wa timu yake, pale alipomuanzisha Hemed Kibopile acheze kama beki
wa kushoto na Hassan Mwasapili asogee mbele
ili kuongeza idadi ya viungo na aweze mara kwa mara kurudi nyuma
kusaidia walinzi, kazi ambayo aliifanya
kwa ufanisi mkubwa. Kwa hiyo Mbeya City walikua na viungo watatu, Mazanda,
Matogoro na Mwasapili, ingawa hata Deus Kaseke nae alikua akiingia ndani
kujaribu kuwasaidia viungo.
![]() |
| MASHABIKI WAKIGOMBEA TIKETI |
Kwa upande wa Simba, walimuweka
mshambuliaji mmoja tu Amisi Tambwe na mabeki halisi waliocheza walikua ni
wawili, Josef Owino na Don Musoti, hivyo
wachezaji saba waliobaki walikua ni
viungo, Henry Josef, Wiliam Lucien, Said Ndemla, Amri Kiemba, Mkude, na hata
Singano na Chanongo pia nao ni viungo
washambuliaji, na kwa jinsi jana wachezaji wa Simba walivyocheza kila mmoja
alikua katika form ya hali ya juu sana na kuwafanya Mbeya City wacheze kwa
nguvu zaidi ili kuweza kuwahimili.
![]() |
| MASHABIKI WA MBEYA CITY |
Jonas Mkude na Said Ndemla walifanya
kazi ngumu sana ya kumzuia Steven Mazanda asianzishe mashambulizi, ingawa mara
kadhaa alifanikiwa kuwatoka na kupiga
pasi kwa washambuliaji wake. Anton Matogoro alikua na kazi ya kucheza na Amri Kiemba, hivyo muda mwingi wa
mchezo alicheza chini ili aweze kumkaba Kiemba na wenzake waliokua wanakuja
kila mara, ana mapafu ya ajabu sana Matogoro, na alicheza vizuri mno.
Mmoja wa wachezaji walionivutia
katika michezo miwili wa Mbeya City na Mtibwa na pia huu wa Simba ni Hemed
Kibopile, ni mlinzi mzuri mno na anatumia akili na nguvu kila inapobidi,
alicheza vizuri sana kumzuia Singano wa Simba, hadi alipopewa kadi ya njano na
kocha kumuondoa ili kuepusha kadi nyingine ya njano. Aliweza kuhakikisha
Singano hana madhara makubwa, ukichukulia Singano alivyo mzuri, hiyo ni kazi
kubwa sana na aliifanya kwa ufanisi.
![]() |
| SHABIKI WA MBEYA CITY |
John Kabanda alicheza kwa tahadhari
kubwa kwani Chanongo alikua katika
kiwango kizuri na alikua akitaka kulazimisha kupita upande wa Kabanda,
mpambano wao ulikua ni mzuri kuutazama, ingawa baadae Chanongo alichoka na
kuanza kupoteza umakini hadi akatolewa. Kabanda kama kawaida yake alipiga krosi
kadhaa langoni mwa goli la Simba lakini nyingi ziliokolewa na walinzi.
Kazi ilikua ni kwa Amisi Tambwe na
Deogratius Julius, Tambwe alikua hatari sana na alipata nafasi kadhaa ambazo
hakuzitumia vizuri ingawa alikuja kufunga goli lakini Deo alimdhibiti na
kumfanya Tambwe mara nyingi kucheza kwa hasira. Deo alikua katulia mno na
kuokoa kwa umakini mkubwa hivyo kuweza kuhimili misukosuko yote iliyokua
ikija langoni mwao.
Yusuf Abdallah alikua akiosha hatari nyingi zilizokua zikija langoni na
ni yeye alliyekua akipambana na hatari
zote zilizowapita mabeki wa pembeni na hata zilizopita katikati, ni mmoja kati
ya mabeki bora sana hapa Tanzania.
Hassan Mwasapili alicheza vizuri alipokua kiungo, lakini baadae
aliporudi kucheza nafasi aliyoizoea ya beki wa kushoto alIcheza vizuri zaidi,
kwani walianzisha tena kombinesheni yao na Deus Kaseke na kufanya mashambulizi
kadhaa dakika za mwisho za mchezo.
![]() |
| MASHABIKI |
Deus Kaseke alicheza sana ndani tofauti
na michezo mingi alivyozoeleka kucheza, hiyo inatokana na Simba kua na viungo
wengi hivyo ikabidi aingie ndani zaidi kuwasaidia viungo wake, na alikua hatari
kila mara anapopata mpira, alipeleka mipira kadhaa kwa washambuliaji wake na
aliweza kuwasaidia vizuri viungo wa timu yake. Mara nyingi alifanikiwa kumtoka
Lucien na kupiga hiyo mipira katikati.
Paul Nonga na hata Mwagane Yeya walikua
na kazi nzito ya kupambana na walinzi warefu wa Simba kina Josef Owino na
Musoti, ingawa ilionekana kuwakaba Nonga na Yeya ni kazi ngumu na
inayohitaji ujasiri, Musoti na Owino walijitahidi kupambana hadi dakika ya
mwisho.
![]() |
| MAMIA YA MASHABIKI WALIOJITOKEZA |
Kwa ujumla mchezo ulikua ni mzuri na wa
kiufundi zaidi, viungo wa Simba walicheza kwa nguvu na akili sana hivyo
kuwafanya wachezaji wa Mbeya City kutumia nguvu zaidi ili kuweza kuwazima
Simba, na kikubwa Mbeya City wanacheza kwa ushirikiano kila idara ndio maana walifanikiwa,
kwani hadi mchezo unakwisha Mbeya City
moja na Simba moja.
PICHA NA MWANDISHI JUNIOR,IMEANDIKWA NA ABDUL SUDI, MBEYA






No comments:
Post a Comment