Monday, 3 March 2014

Kocha mwambusi
BADO TUPO VIZURI

Kocha mkuu wa timu ya Mbeya City, Juma mwambusi amesema timu yake bado iko vizuri pamoja na matokeo waliyopata karibuni.
     Timu hiyo imetoka sare na JKT Oljoro katika mchezo wake wa mwisho, na kabla ya hapo ilipoteza kwa timu ya Coastal Union ya Tanga.

       Akiongelea matokeo hayo kocha Mwambusi amesema “bado nawaamini vijana wangu kwani hadi sasa wako imara na wanajitahidi kwa nguvu zao kuhakikisha tunapata matokeo mazuri, kilichotokea ni hali ya kawaida ya mchezo, hivyo kila ukimaliza mechi moja inatakiwa utazame uliyokosea na kujaribu kuyarekebisha ili katika mchezo unaofuata usirudie makosa hayo hayo”alisisitiza.
KOCHA MWAMBUSI AKITOA MAELEKEZO(picha toka katika mtandao)
     ‘Ukitazama mzunguuko wa kwanza timu ilionekana iko vizuri sana na kila mtu aliifurahia na kuipa sapoti kubwa,  lakini kuna mambo mengi ya kiufundi yametokea hapo katikati,  mfano ligi ilisimama zaidi ya miezi miwili, na kumbuka wakati huo vijana wangu walikua tayari wako juu sana ki mchezo na morali pia ilikua iko juu sana, matokeo yake ligi iliposimama timu nyingine nyingi zilifanya usajili mpya na kurekebisha makosa yao kwa kujitayarisha upya, na sisi pia tukaanza upya kujitayarisha, lakini kumbuka morali lazima inakua imeshuka na kuijenga ni kazi kubwa na inayofanyika taratibu sana, hilo halina ujanja, ndio maana pamoja na mambo mengine madogo madogo, matokeo yanabadilika”aliongeza kocha.
KOCHA MWAMBUSI
         “Mimi binafsi natamani kila siku timu yangu ipate ushindi, na ninajitahidi kila siku kuwafundisha na kurudia kuwafundisha mbinu nyingi na nzuri za kuwafanya wapate ushindi,ninashukuru  wachezaji wangu ni waelewa mno hivyo tuko pamoja kwa kila kitu, wote tunaumia sana na matokeo haya lakini ninachofanya kila siku ni kuwaambia mkifungwa sio mwisho wa dunia, jipangeni ili tuhakikishe tunashinda mchezo unaokuja, wasikate tamaa na kuona kama vile ndio tumefika mwisho wetu, bado tuna nafasi na tutapigana hadi dakika a mwisho” alisisitiza.
    “Sasa hivi tuna wakati mgumu sana maana tunacheza na timu ambazo ziko katika hatari ya kushuka daraja, hivyo nazo zinapania sana zinapocheza na sisi, na pia hata jina letu tulilolijenga nalo linazifaya timu zipanie kufia uwanjani kila zinapocheza na sisi, hivyo kikubwa ninachofanya ni kuwaambia vijana wangu, tupambane hadi dakika ya mwisho na INSHA ALLAH tutashinda mapambano yetu” alimalizia kocha Mwambusi.
     Mbeya city mwishoni mwa wiki hii itacheza na timu ya Rhino toka Tabora.


1 comment:

  1. This comment has been removed by a blog administrator.

    ReplyDelete