Saturday, 29 March 2014

MECHI YA KARNE
Tz Prisons na Mbeya city

                    IMEANDIKWA NA JOEMAN JOH, MBEYA/picha toka vyanzo mbali mbali.
Jumapili  tarehe 30,Machi,2014 kutakuwa na mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania kati ya Tz Prisons dhidi ya Mbeya City. Hiyo ni Mbeya derby kwani wote ni watoto wa jijini Mbeya na hata mitaa zinapotoka timu hizi siyo mbali.


       Mchezo huu unazikutanisha timu mbili zikiwa na malengo tofauti, City inataka kuzikimbilia YANGA na AZAM kwenye kilele cha ligi, wakati Tanzania Prisons inakimbia kusalimisha roho yake, kwani ipo katika hatari ya kushuka daraja.
TZ PRISONS

     Wakati City wakiwa nafasi ya tatu katika msimamo waligi, Prisons hadi sasa iko nafasi ya 10 kati ya timu 14. Lakini ukiondoa kipigo cha kushtukiza walichokipata toka kwa Yanga, wapo vizuri sana ki uchezaji na ari ya kimchezo.

  Toka mzunguuko wa pili uanze Prisons wamepoteza michezo miwili tu, kwa Kagera na Yanga, na zote wamepoteza ugenini, lakini zilizobaki wamefanya vizuri.

     Upande wa pili City  imeshinda mechi zake zote mbili za mwisho dhidi ya RHINO (Sokoine) na dhidi ya JKT Ruvu(Chamazi).Kutokana na matokeo hayo na yale ya mechi ya kwanza baina yao ambapo City walishinda 2-0 yanaleta taswira ya jinsi gani mechi hii itakavyokuwa ngumu...
MBEYA CITY

    Kingine kinacholeta ugumu wa mechi ni malengo yao pamoja ufundi wa makocha Juma Mwambusi na David Mwamwaja ambaye kaibadilisha Prison kuwa timu inayocheza vizuri tofauti na awamu ya kwanza..

    City wanaoongozwa na kocha Juma Mwambusi, wanacheza mpira wa kasi na wanatumia sana walinzi na viungo wao wa pembeni, John Kabanda,Hassan Mwasapili, Deus kaseke na Peter Mapunda kuanzisha mashambulizi, pia wana wafungaji wengi wazuri kwani hadi sasa tayari kuna washambuliaji wanne wamepokezana kufunga magoli, Mwegane Yeya, Peter Mapunda,Richard Peter(ambae ni majeruhi)  na Saad Kipanga, pia Paul Nonga ni mpiganaji mzuri sana na ni tatizo kwa kila beki anaekutana nae. washambuliaji hao ni wazuri sana kwa kucheza mipira ya juu.
KOCHA WA MBEYA CITY, JUMA MWAMBUSI

    Tz Prisons walio chini ya kocha mzoefu David Mwamwaja, wao wanacheza mchezo wa pasi nyingi na hua wanawatumia wachezaji wao wa katikati, Jimy Shoji na Omega Seme (inasemekana alikataa kucheza mchezo na Yanga, kwa vile tayari alikua ameweka mkataba wa kuichezea timu hiyo msimu ujao) kupeleka mashambulizi mbele ambapo wanamtegemea Peter Michael mwenye magoli zaidi ya nane msimu huu kufunga. Pia wana beki wa kulia Salum Kimenya ambae ni  mzuri sana wa kupanda na kupiga krosi.
DAVID MWAMWAJA, KOCHA WA TZ PRISONS

      Timu zote zina walinzi wazuri sana wa katikati, Prisons yupo Lugano Mwangama na Nurdin Chona ambao wanatumia akili na nguvu nyingi kuwadhibiti washambuliaji wa timu pinzani, wakati Mbeya City wana uhakika na mabeKi wao wa kati, Yohana Morris, Yusuf Abdallah pamoja na Deo Julius ambao shughuli yao mara zote inakua ni kubwa na ya uhakika.
FRANCIS CASTRO WA MBEYA CITY AKIWAA NA JIMY SHOJI WA TZ PRISONS
       Kwa ujumla mchezo unatarajiwa kuwa wa ushindani zaidi, hatutarajii kuona mchezo wa upande mmoja au wa kubebana, kwani kwa jinsi timu hizi mbili zilivyo, kuna uadui mkubwa wa ndani ya uwanja ingawa mchezo ukiisha wachezaji wengi ni marafiki. Ukitazama asilimia kubwa ya hawa wachezaji wamecheza pamoja toka utotoni, wamkekuja kutengana tu pale wengine wanacheza  City na wengine Prisons.

Kwa mashabiki wa timu hizo, tunategemea kutakua na kuzomeana, kutaniana na hata kejeli za hapa na pale lakini hizo ndizo zinazofanya mchezo upendeze zaidi, hatutegemei kutokea fujo kama zilizotokea walipokutana mzunguuko wa kwanza.
       KILA LA KHERI TZ PRISONS NA MBEYA CITY.






No comments:

Post a Comment