Tuesday, 16 September 2014

 Ivo mapunda
KIPA ASIYECHUJA TANZANIA

   
Ukiongelea makipa bora kabisa waliowahi kutokea hapa nchini na bado wanatamba huwezi kuacha kumtaja Ivo Mapunda, pamoja na kua alianza kucheza mpira muda mrefu, lakini hadi sasa ubora wake unazidi kuongezeka.  Ana uwezo wa kucheza mipira ya aina yote, ya juu na ya chini, pia umbo lake kubwa linamsaidia hata katika ile mipira ya kupambana na ya krosi
.  kizuri zaidi ana uwezo mkubwa  wa kucheza penati, na kikubwa anachowazidi makipa wengine ni jinsi anavyojua kuanzisha mashambulizi kila anapodaka mpira.
IVO MAPUNDA

     Si ajabu kuona mashabiki wa timu pinzani wakiwa na wasiwasi kila anapokua golini, hua wanafikia hadi kuwaza kwamba taulo analopenda kuliweka katika nyavu lina nguvu za giza,zinazomsaidia kulinda lango lake.  Ingawa ki ukweli ni imani zao tu kwa kua mara nyingi wanashindwa kupata matokeo anapokua golini.
IVO AKIWA NA TAULO LAKE

Ana uzoefu mkubwa sana, na kilichomsaidia  ni kwamba alianza kucheza soka  akiwa na umri mdogo hivyo amekutana na makipa na makocha wa aina nyingi katika timu tofauti alizochezea, amecheza ligi kubwa katika nchi tatu tofauti na kwa mafanikio.
IVO MAPUNDA AKIWA NA SHAABAN KADO NA JUMA KASEJA
  Alizaliwa katika sehemu inayoitwa Kisa Ushirika , Tukuyu Mbeya na kusoma katika shule ya msingi hapo hapo Kisa aliposoma hadi darasa la sita akahamia Mafinga katika shule ya Nyololo. Baadae akajiunga na shule ya sekondari ya ufundi  ya Ifunda. Na hapo alichukua masomo ya motorvehicle  mechanics, na alipomaliza alifaulu vizuri na kuchaguliwa kwenda katika chuo cha ufundi Mtwara.
 Hakuenda huko chuoni, kwani muda huo tayari akili yake ilikua imezama katika soka.

     Alirudi nyumbani  Mbeya na kuanza kucheza katika madaraja ya chini, akianzia na timu ya Mpuguso Stars ya Ushirika Tukuyu.
   Mfadhili wa Tukuyu Stars wakati huo akiitwa Rampa alimchukua na kumpeleka Tukuyu Stars na hapo alidumu miaka miwili kabla hajachukuliwa na timu ya Tz Prisons, na akawa ni askari kamili wa jeshi la Magereza, akiwa na cheo cha koplo.
KOPLO IVOMAPUNDA 

    Akiwa Tz Prisons alikaa miaka sita kisha akahamia Moro United ya Morogoro. Hapo pia alikaa miaka miwili na kuhamia katika timu ya Yanga.
   Baada ya miaka mitatu akaondoka katika timu hiyo na kwenda kuheza mpira a kulipwa katika timu ya st George ya Ethiopia, kisha akarudi nyumbani Tanzania na kujiunga na African Lyon ambapo pia alikaa miaka miwili na kisha  akaamua kutoka tena na kwenda Kenya katika timu ya Bandari Mombasa.
        Alikaa miezi sita na  akachukuliwa na Gor Mahia ya hapo hapo Kenya alikokaa miaka miwili, na ndipo klabu ya Simba  ikaamua kumchukua na ndio anaitumikia hadi sasa.
RAISI SHEIN WA ZANZIBAR AKISALIMIANA NA WACHEZAJI WA SIMBA KABLA YA MCHEZO NA KMKM

  Akiongelea kuhusu soka  Ivo alisema "kikubwa katika soka ni kujituma na kujaribu kujiepusha na mambo ambayo hayaendani na soka, ninashukuru nimecheza kwa muda mrefu kwa vile ninajua thamani yangu, hivyo ninajitunza na kufanya yale ambayo yanatakiwa kufanywa na mchezaji. Nimeanza kucheza nikiwa na umri mdogo sana, hivyo nimekutana na mambo mengi katika hii miaka niliyocheza. hakuna njia ya mkato, ni kufanya mazoezi kila siku hiyo ndio silaha ya mcheza soka."
   " sasa hivi nipo Simba na matayarisho tunayofanya ni mazuri, hivyo na mategemeo yangu ni kwamba timu yetu itafanya vizuri zaidi kaitika msimu huu"




No comments:

Post a Comment