Saturday, 20 September 2014

KARIBUNI MBEYA CITY INAWASUBIRI

KARIBUNI
MBEYA CITY INAWASUBIRI
        Msimu mpya wa ligi umefika, Mbeya City inaanzia pale pale ilipoishia msimu uliokwisha.
Ilishika nafasi ya tatu, hakuna aliyetegemea hilo,  lakini liliwezekana,  na sasa hivi inatarajia kwenda juu zaidi. Ni kazi ngumu,  ukichukulia timu zote zitakua zinaipania Mbeya City, kwani wanajua wakifanya makosa muziki wa City ni mkubwa , wataadhirika.
    Lakini nayo matayarisho yake si haba, ingawa walifungwa na Vipers lakini sio kipimo kwamba hawako vizuri, timu imetulia na iko vizuri zaidi ya msimu uliokwisha. Kocha mkuu wa timu hiyo Juma Mwambusi  anafurahia kikosi chake kilivyo “ nashukuru Mungu timu iko salama na imefanya mazoezi ya kutosha, tumejitahidi kurekebisha makosa madogo madogo ambayo yalitugharimu msimu uliopita, hivyo sasa hivi tuko imara zaidi”
KOCHA MWAMBUSI
    Alipoulizwa makosa yenyewe ni kama yapi akasema “ mfano tulicheza na Azam katika mzunguuko wa kwanza Dar, tayari tulikua tunaongoza  3-2, na dakika zilikua zimekwisha. Mchezaji wetu akawa kaumia, ila mpira tulikua nao sisi, wachezaji wangu hawakua na uzoefu kwani waliendelea kushambulia kwani waliona kuna nafasi ya kupata bao la nne, lakini matokeo yake  Azam walipookoa wakafanya shambulizi kali counter attack na kupata bao la kusawazisha” aliongea kwa masikitiko “ wangekua na uzoefu, wangeutoa mpira nje ili mwenzao atibiwe na kisha mchezo ungepoa na dakika zingemalizika kwa ushindi, lakini ndio hivyo, sasa hivi wana uzoefu wa kutosha makosa kama hayo sidhani kama yatatokea tena”
       “ Kitu ninachofurahia, hakuna mchezaji aliyeondoka, wote wapo na pia tumeongeza nguvu kwa kumleta Themi Felix toka Kagera  akasaidiane na kina Mwegane kule mbele, tunajua uzoefu wake katika ligi utatusaidia kupata matokeo mazuri, maana ni mfungaji mzuri sana, naweza sema ni mmoja kati ya wafungaji bora Tanzania. Pia tumemuongeza kiungo Peter Mwalyanzi kutoka Mgambo JKT.
 Alipoulizwa kama anafikiria kupata ubingwa sasa hivi akasema “ hapana, siwezi kuahidi kitu kama hicho, msimu uliopita hatukuahidi kitu na tazama tulipofikia, na sasa hivi hatuahidi kitu, ila tuna uhakika tutafanya vizuri sana,  Hua napenda kuichukulia kila timu ninayokutana nayo kwa uzito mkubwa, hivyo kwangu mimi kila mchezo ni fainali, napenda niwe najipanga kwa mchezo unaofuata, najua tutafika kila mmoja anapotamani kufika”
     


No comments:

Post a Comment