Sunday, 20 April 2014

TZ PRISONS YA UKWELI

         Ligi kuu ya soka Tanzania bara imemalizika kwa Azam Fc kuchukua nafasi ya kwanza huku Yanga ikiwa ya pili na timu ngeni katika ligi ya Mbeya City ikiwa nafasi ya tatu.

      Haukua msimu mzuri sana kwa timu ya Tz Prisons, kwani  hadi dakika ya mwisho ilikua ikipigania roho yake ili isishuke daraja. Ilianza ligi hiyo kwa kusua sua lakini mzunguuko wa pili ilikua ni moto wa kuotea mbali.
  Ilifanikiwa kubaki katika ligi hiyo baada ya kuifunga timu ya Ashanti kwa goli moja kwa bila, katika mchezo uliochezwa uwanja wa jamhuri Morogoro. Mchezo huo ulihudhuriwa na mashabiki wengi kutoka jijini Mbeya waliosafiri ili kuipa sapoti timu yao.
mashabiki waliokuwa wakiishangilia Tz Prisons
     Goli hilo muhimu lilifungwa na mshambuliaji wake hatari Peter Michael, ambae kwa msimu huu ameonyesha kua ni mmoja kati ya washambuliaji wenye uhakika wa kufunga katika ligi hiyo.
    Ukitazama kwa haraka haraka unaweza kusema Tz Prisons hawakua na uwezo ndio maana wakawa katika  nafasi hiyo, lakini si hivyo. Kwani ni moja kati ya timu zilizoonyesha kiwango cha hali ya juu sana na cha ushindani. Ila kilikua na matatizo madogo madogo ambayo walichelewa kuyapatia ufumbuzi.
mashabiki wakipongezana baada ya kunusurika kushuka darajaAdd caption
       Katika mchezo wa mwisho dhidi ya Ashanti, walionyesha kiwango cha juu kiasi kila mtu aliyekuwepo uwanjani alishangaa ni kwa nini wanapigania kushuka daraja badala ya kuwa katika nafasi nne za juu.
        “ Tatizo kubwa la kwanza lililowakuta Tz Prisons ni kwamba walichelewa sana kubadilisha benchi la ufundi, kocha Jumanne Chale hana uwezo wa kufundisha timu za madaraja ya juu, ndio maana hata alipokwenda Rhino amewashusha daraja” aliongea  Fernad Daudi Mwakilembe, mmoja wa mashabiki waliokua wakiishangilia  timu ya Prisons uwanjani Jamhuri.  
Ally Mlagha(kushoto) na Fernard Daudi Mwakilembe wakiwa na mlinzi wa Tz Prisons,Nurdin Chona.
 
     “hakua na mipango ya uhakika kuifanya timu icheze vizuri , lakini toka alipokuja David Mwamwaja timu imebadilika na hata uchezaji na ari kwa wachezaji imeongezeka sana” aliendelea kuongea.
       Katika mchezo huo, goli pekee lilipatikana kipindi cha pili na kuwafanya Ashanti wapate certificate ya kucheza daraja la kwanza.
  Nae Ally Mlagha aliyesafiri toka Mbeya kuipa nguvu timu hiyo alisema “unajua Ashanti wametengenezewa sana mazingira ya kubaki ligi kuu. Lakini uwezo hawana, ukitazama hata jinsi mchezo wao na Simba ulivyobadilishwa na kusogezwa mbele ili tu wajue matokeo ya timu nyingine utaona kua walikua wakitaka Ashanti ibaki, na hata uamuzi wa kusema mchezo huo uchezewe Morogoro, ilikua ni kutengeneza mazingira tz prisons icheze bila mashabiki wake, kwa maana michezo yote miwili dhidi ya Ashanti wamecheza ugenini”.
        Prisons waliwazidi kila idara Ashanti, na kama wangekua makini wangeweza kupata magoli mengi zaidi. Ukuta wa timu hiyo uliokua ukiongozwa na Nurdin Chona, beki mwenye kujituma na kujua vilivyo kukabiliana na washambuliaji tofauti,  ulikua imara na kuweza kuwadhibiti vilivyo washambuliaji hatari wa Ashanti wakiongozwa na mshambuliaji mwenye kasi na akili Ally Kabunda.
kocha David Mwamwaja akingea na waandishi baada ya mchezo na Ashanti uwanja wa Jamhuri Morogoro.
   Baada ya mchezo huo kocha wa Tz Prisons, David Mwamwaja alisema amefurahishwa na matokeo ya mchezo huo na kwa sasa wanaanza kujipanga ili msimu ujao timu iwe na ubora zaidi ya ulioonekana mwaka huu. " ligi imekwisha, tunakwenda kutazama ni wapi tulikosea ili msimu ujao tujue jinsi ya kurekebisha na kuboresha zaidi, kikubwa ninapenda kuwapongeza sana wachezaji wangu, kwani kazi waliyofanya ni kubwa na ngumu sana" alimalizia kocha huyo aliyeisaidia sana Tz Prisons kubaki ligi kuu.


    

1 comment: